MLANGO WA TWAHARA-05

DAMU YA MNYAMA MWENYE KULIWA


Mjadala kuhusu damu hii, ni kama mjadala kuhusu damu ya mwanadamu kwa upande wa kutokuwepo dalili juu ya unajisi wake. Kwa hivyo inaambatana na utwahara wa asili.
Kusema kuwa ni twahara kunaungwa mkono vilevile na:
Yaliyoelezewa na Ibnu Masoud, amesema: "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali mbele ya Ka’abah, na ilhali Abuu Jahli na marafiki zake wamekaa. Pale walipoambiana: Ni yupi kati yenu atakayewaendea ngamia wa
akina fulani, akakusudia taka zake, damu zake, na miji yake (wombs), kisha akamsubiri mpaka anaposujudu, halafu akamwekea mabegani mwake? Basi mwovu wao akachomoka haraka, na aliposujudu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyaweka kati ya mabega yake, na Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam alitulia tuli katika sijdah, na wao wakacheka. (Hadiyth Sahihi: Al-Bukhaariy (240) na Muslim (1794))

Na lau kama damu ya ngamia ingelikuwa ni najisi, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliitupa (angeliidondosha) nguo yake, au angeliikatisha Swalah yake.

Na imethibiti kwa njia sahihi kwamba Ibnu Mas’uud aliswali na ilhali katika tumbo lake kuna taka na damu ya ngamia aliowachinja, na wala hakutawadha.
 (Isnadi yake ni sahihi: Muswannaf Abdur-Raaziq (1/25), na Ibnu Abuu Shaybah (1/392))

Na ingawa tukiona pokezi hili "athar" linaweza kufanyiwa mvutano katika kutolea ushahidi juu ya utwahara wa damu ya mnyama, kwa vile Ibnu Mas’uud hakuwa akiona kwamba utwahara wa mwili na nguo ni sharti ya kusihi Swalah, bali anaona kuwa ni jambo linalopendeza (mustahab).


Ninasema (Abuu Maalik): Lau kama imethibiti kwa ijmaa kwamba damu ni najisi, basi hatutaziangalia dalili za waliofuatia baadaye. Na kama haikuthibiti, basi asili ni utwahara na sisi hatuhitajii dalili hizo. Na lililodhihiri kwangu - baada ya kuchagua kauli (isemayo kuwa) damu ni twahara kwa kipindi cha miaka kumi - ni kwamba ijmaa katika suala imethibiti. Ijmaa hii imenukuliwa na Maulamaa wengi na hakikuthibiti chenye kuitengua. Na nukuu ya juu zaidi kati ya hizo ni yale yaliyonukuliwa toka kwa Imaam Ahmad, kisha yale aliyoyanukuu Ibn Hazm, kinyume na yule aliyedhani kwamba madhehebu yake yanasema kwamba damu ni twahara!! Na kati ya niliyoyafahamu katika hilo ni:

Ibnu Al-Qayyim katika "Ighaathat Allahafaan" (1/420) amesema:

Ahmad aliulizwa: "Je, damu na usaha kwako ni sawasawa"? Akasema: "Hapana, watu hawakuhitilafiana kuhusu damu".

Na alisema mara moja: "Usaha kwangu ni afadhali kuliko damu…".

Na imenukuliwa toka kwa Ibnu Hazm katika "Maraatib Al-Ijmaa": "Kukubaliana Maulamaa juu ya unajisi wa damu".

Vile vile Al-Haafidh katika "Al-Fat-h" (22/420) amekunukuu kukubaliana huko.

Na Ibnu Abdul-Barri katika "At-Tamhiyd" (22/230) anasema:


"Na hukumu ya kila damu ni kama damu ya hedhi, isipokuwa damu kidogo husamehewa kwa vile Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameweka sharti ya unajisi wa damu kuwa iwe ni yenye kuchuruzika, na hapo inakuwa ni uchafu, na uchafu ni najisi. Na hii ni ijmaa ya Waislamu kwamba damu yenye kuchuruzika ni uchafu na najisi..".

Na Ibnu Al-Araby katika "Ahkaam Al-Qur-aan" (1/79) anasema:

"Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni haramu na ni najisi kwa kinacholiwa na kisichopatiwa manufaa. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameiainisha hapa kwa kuifanya ni yoyote ile (mutwlaq), na katika Surat Al-An 'Aam Ameiainisha kwa kuiwekea mpaka (muqayyad) ile tu ya kuchuruzika. Na Maulamaa kwa ijmaa hapa, wameichukulia damu yoyote wakaiacha iliyowekewa mpaka….".


Na An-Nawawy katika Al-Majmu’u (2/576) amesema:
"Na dalili juu ya unajisi wa damu zinatiliana nguvu zenyewe kwa zenyewe, na mimi sijui kama kuna hitilafu yoyote toka kwa Muislamu yeyote ila tu yale aliyoyaelezea mtunzi wa Al-Haawiy toka kwa baadhi ya Maulamaa wa tawhiyd. Amesema kuwa ni twahara, lakini Maulamaa wa tawhidi maneno yao hayachukuliwi katika ijmaa au mahitalifiano…".


Ninasema (Abuu Maalik): Ninalolipa nguvu na uzito ni kuwa damu ni najisi kwa kuthibiti ijmaa mpaka inukuliwe toka kwa Imaam mwingine atakayempiku Imaam Ahmad – (Allaah Amrehemu) – kwa kusema kuwa damu ni twahara. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

Baadhi Ya Adabu Za Kustanji


Kati ya adabu ambazo inatakikana mtu ajipambe nazo wakati wa kustanji ni:

1- Asistanji kwa mkono wa kulia;
Ni kutokana na Hadiyth ya Abuu Qataadah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ﻻ‌ ﻳﻤﺴﻜﻦ ﺃﺣﺪﻛﻢ ﺫﻛﺮﻩ ﺑﻴﻤﻴﻨﻪ ﻭﻫﻮ ﻳﺒﻮﻝ، ﻭﻻ‌ ﻳﺘﻤﺴﺢ ﻣﻦ ﺍﻟﺨﻼ‌ﺀ ﺑﻴﻤﻴﻨﻪ، ﻭﻻ‌ ﻳﺘﻨﻔﺲ ﻓﻲ ﺍﻻ‌ﻧﺎﺀ))

((Asikamate kabisa mmoja wenu uume wake kwa mkono wake wa kulia wakati wa kukojoa, wala asijisafishe haja kwa mkono wake wa kuume, wala asipumulie ndani ya chombo)). (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (153), Muslim (267), na wengineo)

Na imepokelewa toka kwa Salmaan, amesema: “Mtu mmoja aliniambia: “Hakika mwenzenu huyu anawafundisheni hata kwenda haja kubwa”. Akasema (Salmaan): “Ndiyo. Ametukataza kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, ametukataza kustanji kwa mikono yetu ya kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu”. (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (262), Abuu Daawuud (7), At-Tirmidhy (16), An-Nasaaiy (1/16))


2- Asiuguse utupu kwa mkono wake wa kulia

Ni kwa Hadiyth ya Abuu Qataadah iliyotangulia.


3- Ausugue mkono wake ardhini (kwenye udongo), au auoshe kwa sabuni na mfano wake baada ya kustanji

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiingia msalani, nilikuwa nikimpelekea maji katika kijindoo kidogo, halafu hustanji na kisha huupangusa mkono wake juu ya ardhi”. (Hasan kwa nyingine: Imetolewa na ….(45), Ibnu Maajah (678), An-Nasaaiy (1/45), na angalia katika kitabu cha “Al-Mishkaat” (360))

Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Maymuna isemayo: “Kisha Mtume alijimwagia maji juu ya utupu wake, akauosha kwa mkono wake wa kushoto, kisha akaupiga mkono wake juu ya ardhi, halafu akauosha”. (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (266), na Muslim (317))

4- Aunyunyizie utupu wake na nguo yake maji baada ya kukojoa ili kuondosha shaka na wasiwasi

Imepokelewa na Ibn ‘Abbaas kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha mara moja, halafu akaunyunyizia maji utupu wake.
 (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ad-Daaramy (711), Al-Bayhaqy (1/161). Na Al-Albaany katika kitabu cha “Tamaam Al-Minnah” uk. 66 anasema kuwa sanadi yake ni sahihi juu ya sharti ya Mashaykh wawili)



NAMNA MGONJWA WA KICHOCHO AU MFANO WAKE ANAVYOSTANJI

Aliyepatikana namtihani wa kupatwa na kichocho, atastanji na kutawadha kwa kila Swalah. Na vile vinavyomchuruzika havina madhara yoyote kwake madhali wakati wa Swalah nyingine haujaingia. Na hii ndiyo kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa. Kauli hii imesemwa na Abuu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ishaaq, Abuu Thawr na wengineo.

Aliyepata mtihani wa ugonjwa huu, atakuwa na hukumu ya damu ya istihaadha. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelizungumzia hilo aliposema:

((ﺍﻧﻤﺎ ﺫﻟﻚ ﻋﺮﻕ، ﻭﻟﻴﺴﺖ ﺑﺎﻟﺤﻴﻀﺔ، ﻓﺎﺫﺍ ﺃﻗﺒﻠﺖ ﺍﻟﺤﻴﻀﺔ ﻓﺪﻋﻲ ﺍﻟﺼﻼ‌ﺓ، ﻓﺎﺫﺍ ﺫﻫﺐ ﻗﺪﺭﻫﺎ، ﻓﺎﻏﺴﻠﻲ ﻋﻨﻚ ﺍﻟﺪﻡ ﻭﺻﻠﻲ))
((Hakika hiyo ni damu ya mshipa na wala si damu ya hedhi. Na hedhi inapokujia, basi acha kuswali. Muda wake unapomalizika, oga ujitwaharishe na damu, kisha swali)). (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (228), Muslim (333) na wengineo)

Na kwa upande wa Al-Bukhaariy, amesema: Na akasema Ubayy: “Kisha tawadha kwa kila Swalah mpaka uje wakati huo”.
 (Hii inawezekana ikawa ni Hadiyth Marfu’u kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inawezekana pia ikawa ni kauli ya ‘Urwah bin Az-Zubayr mpokezi wa Hadiyth toka kwa ‘Aaishah. Aliwajibu kwa kauli hiyo wanawake waliomuuliza kuhusu suala hilo kama ilivyo kwa Ad-Daaramy (1/199))


Ninasema (Abuu Maalik): Hukumu hii bila shaka ni kwa mwenye udhuru kwa ajili ya kumwondoshea uzito. Na hakuna shaka kuwa sheria imekuja kwa ajili ya kuuondoshea umma uzito. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

« ﻳﺮﻳﺪ ﺍﻟﻠﻪ ﺑﻜﻢ ﺍﻟﻴﺴﺮ ﻭﻻ‌ ﻳﺮﻳﺪ ﺑﻜﻢ ﺍﻟﻌﺴﺮ»

«Mwenyezi Mungu Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito»
(Surat Al-Baqarah : 185)

Maalik na wengineo wanaona kwamba haimpasi mgonjwa huyo kustanji wala kutawadha ila tu kama atapata hadathi nyingine.


Ninasema (Abuu Maalik): Ama kutokupasa kutawadha kwa kila Swalah endapo kama hajapata hadathi, huenda hilo lina mwono kwa wale waliotia udhaifu katika kuongezwa neno “na utawadhe kwa kila Swalah” katika Hadiyth iliyotangulia. Na lenye nguvu hapa ni kutawadha kwa kila Swalah kama itakavyokuja katika mlango wa hedhi. Ama kutopasa kustanji, basi hilo halina cha kuzungumziwa, kwani anaweza kutokwa na kinacholazimisha kustanji na akawa na wasaa wa kufanya hivyo kabla ya Swalah bila ya uzito wowote. Anachosamehewa ni kile tu kinachomtoka wakati wa Swalah kwa ajili ya kuepuka uzito.

Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

ADABU ZA KUKIDHI HAJA


Mwenye kutaka kukidhi haja ndogo au kubwa, inatakikana ajipambe kwa adabu zifuatazo:

 1. Ajisitiri na ajiweke mbali na watu na hasa hasa uwandani.

Imepokelewa na Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake), amesema: “Tulitoka na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hafiki uwandani, isipokuwa hupotea asionekane”.
 (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (2), Ibn Maajah (335) na tamko ni lake)

2- Asiwe na kitu chenye utajo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu
 (Angalia katika vitabu cha “Al-Majmu’i” (2/87), Al-Mughniy (1/227) na Al-Awsat (1/342))


Ni kama vile pete iliyotiwa nakshi ya Jina la Allaah na vinginevyo. Hii ni kwa vile kulitukuza Jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu ni jambo ambalo kidini linajulikana na wote. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

((ﺫﻟﻚ ﻭﻣﻦ ﻳﻌﻈﻢ ﺷﻌﺎﺋﺮ ﺍﻟﻠﻪ ﻓﺎﻧﻬﺎ ﻣﻦ ﺗﻘﻮﻯ ﺍﻟﻘﻠﻮﺏ))

«Ndivyo hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa moyo» (Surat Al-Hajj : 32))

Hii ni kwa yaliyopokelewa toka kwa Anas kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiivua pete yake anapoingia msalani. (Hadiyth dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na Ibnu Maajah. Al-Albaaniy amesema kuwa ni dhaifu)
 Lakini hii ni Hadiyth Munkar iliyotiwa doa.

Na linalojulikana ni kwamba pete ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa imetiwa nakshi iliyoandikwa “Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu”. (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5872), Muslim (2092) na wengineo)

Ninasema (Abuu Maalik): “Ikiwa pete hii au mfano wake imesitiriwa kwa kitu kama kuwekwa mfukoni au sehemu nyingine kama hiyo, basi itajuzu kuingia nayo. Ahmad bin Hanbal anasema: “Akitaka ataifumbata katika kiganja chake”.
Ikiwa atahofia kupotea kama ataiacha nje, basi itajuzu kuingia nayo kwa vile imelazimu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.


3- Apige BismiLlaah na ajilinde kwa Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia msalani

Atafanya hivi kama ataingia sehemu iliyojengwa (choo). Lakini kama itakuwa ni uwandani, basi atafanya hivyo wakati anapoinyanyua nguo yake. Hii ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((ﺳﺘﺮ ﻣﺎﺑﻴﻦ ﺍﻟﺠﻦ ﻭﻋﻮﺭﺍﺕ ﺑﻨﻲ ﺁﺩﻡ ﺍﺫﺍ ﺩﺧﻞ ﺃﺣﺪﻫﻢ ﺍﻟﺨﻼ‌ﺀ ﺃﻥ ﻳﻘﻮﻝ: ﺑﺴﻢ ﺍﻟﻠﻪ))

((Sitara iliyoko kati ya jini na utupu wa wanaadamu anapoingia mmoja wao msalani, ni kusema BismiLlaah)). (Al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth Sahihi. Imetolewa na At-Tirmidhiy na Ibnu Maajah. Angalia kitabu cha “Swahyhu Al-Jaam’i” (3611))

Na imepokelewa na Anas (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoingia msalani husema:

))ﺍﻟﻠﻬﻢ ﺍﻧﻲ ﺃﻋﻮﺫ ﺑﻚ ﻣﻦ ﺍﻟﺨﺒﺚ ﻭﺍﻟﺨﺒﺎﺋﺚ((

((Ewe Mola! Hakika mimi ninajilinda Kwako na majini wa kiume na majini wa kike)).
 (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (142) na Muslim (375))


4- Atangulize mguu wa kushoto wakati wa kuingia, na mguu wa kulia wakati wa kutoka

Abuu Maalik: Sikupata katika hili matini husika toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Ash-Shawkaaniy amesema katika “As-Saylu Al-Jarraar” (1/64): Ama kutanguliza mguu wa kushoto wakati wa kuingia na mguu wa kulia wakati wa kutoka, basi hili lina hekima yake. Ni kuwa vitu vitukufu huanziwa kwa kulia na visivyo vitukufu huanziwa kwa kushoto. Na bila shaka yenye kuonyesha hilo yamekuja katika sentensi….”


5- Asielekee Qiblah au kukipa mgongo wakati anapokaa kukidhi haja
5- Asielekee Qiblah au kukipa mgongo wakati anapokaa kukidhi haja

Ni kwa Hadiyth ya Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyepokea toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), amesema:

ﺍﺫﺍ ﺃﺗﻴﺘﻢ ﺍﻟﻐﺎﺋﻂ ﻓﻼ‌ ﺗﺴﺘﻘﺒﻠﻮﺍ ﺍﻟﻘﺒﻠﺔ ﻭﻻ‌ ﺗﺴﺘﺪﺑﺮﻭﻫﺎ، ﻭﻟﻜﻦ ﺷﺮﻗﻮﺍ ﺃﻭ ﻏﺮﺑﻮﺍ

((Mnapokwenda haja kubwa, msikielekee Qiblah wala msikipe mgongo, bali elekeeni mashariki au magharibi)).

Abuu Ayyuub anasema: “Tukafika Shaam, tukakuta vyoo vimejengwa kuelekea Ka’abah, tukawa tunakiepa na kumwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu maghfira”. (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (394), Muslim (264) na wengineo)


Lakini hata hivyo, imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar kwamba amesema: “Siku moja nilipanda juu ya paa la nyumba yetu, nikamwona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya matofali mawili akikidhi haja na ilhali ameelekea Baytul Maqdis”.
 (Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (145), Muslim (266) na wengineo)

Na ikiwa ameelekea Baytul Maqdis na yeye yuko Madina, basi atakuwa ameipa mgongo Ka’abah!!

Ninasema (Abuu Maalik): Na ili tuzifahamu Hadiyth hizi mbili, hebu tuziangalie kauli nne mashuhuri za Maulamaa
 (An-Nawawy amezitaja katika kitabu cha “Al-Majmu’i” (2/82). Al-Haafidh ameziongeza kauli nyingine tatu katika kitabu cha “Al-Fath (1/296))
1- Ni kuwa katazo la kuelekea Qiblah na kukipa mgongo ni kwa hali zote sawasawa ikiwa ndani ya jengo au uwandani.

Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Ahmad na Ibnu Hazm. Shaykh wa Uislamu pia ana msimamo huu. Ibnu Hazm amelinukulu hili toka kwa Abuu Hurayrah, Abuu Ayyuub, Ibn Mas’ud na Suraaqah bin Maalik. Pia amepokea toka kwa Atwa’a An-Nakh’i, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy na Abuu Thawr. (Al-Muhallaa (1/194), Al-Fath (1/296), Al-Awsat (1/334), As-Saylu Al-Jarraar (l/69) na Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyat (8))
 Wametoa hoja yao kwa kuitumia Hadiyth ya Abuu Ayyuub iliyotangulia.

2- Ni kuwa katazo hilo linahusiana na sehemu wazi tu lakini si ndani ya jengo.

Hili limesemwa na Maalik na Ash-Shaafi’iy. Kwa kauli yao hii, wao wamepitia mkondo wa kukusanya baina ya dalili mbili. Wamesema: “Kanuni isemayo “Kauli hutangulizwa kabla ya kitendo”, bila shaka hutumiwa katika hali ya kuthibiti umahususi, na umahususi huo hauna dalili yoyote”.


3- Ni kuwa inajuzu kukipa mgongo Qiblah lakini haifai kukielekea.Hili limehadithiwa toka kwa Abuu Haniyfah na Ahmad, wakiuchukulia udhahiri wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar na Hadiyth ya Abuu Ayyuub