MADHARA YA USHIRIKINA  Sehemu ya 1.

Msomaji Wangu Mpendwa
Assalaam Alaykum,


Kama ilivyo ada na desturi nina mshukuru Allah Muumba wa Mbingu na Ardhi kwa kutuwezesha kuwa pamoja tena katika blog yetu hii tukijifunza na kukumbushana mambo mbali mbali yahusuyo maisha yetu ya dunia na akhera. pia namtakia ziada ya rahma na amani Mtume Muhammad S.A.W na Aali zake na Masahaba wake na wote watakaowafuata kwa wema mpaka siku ya hukumu.


Leo nimependelea kutumia fursa hii kukumbusha juu ya madhara ya kujihusisha na vitendo vya ushirikina, ushirikina upo wa namna mbalimbali kuna ushirikina wa kuabudu asiyekuwa Allah ambaye ni Mungu wa pekee asiyefanana na yeyote wala chochote na kuna ushirikina unaotumika kwenye harakati za maisha ya kila siku ya mwanadamu kama vile wa kwenye matibabu,kinga,kipato,ndoa kupata mume au mke,kupanda vyeo makazini utakuta watu wanavaa mahirizi n.k ikumbukwe kuwa aina zote za ushirikina ni mbaya na mtendaji wake iwapo atakufa bila ya kutubu na kumuomba msamaha muumba wake kuna hatari kubwa ya kudumu motoni, mungu atukinge nao.
Leo nitazungumzia aina hii ya ushirikina  ambapo katika sehemu hii ya 1. tutaangalia madhara yanayomkabili Mshirikina mbele za Muumba.

                                kuchinja kwa ajili ya mashetani au mizimu ni 
katika vitendo vya kishirikina


Ndugu Msomaji,

Ushirikina ni katika vitendo alivyoviharamisha ALLAH S.W.T na sote tunajua kuwa Mtume Muhammad S.A.W na Mitume wenzake wote ni miongoni mwa waja vipenzi mbele za ALLAH S.W.T  ni wasafi wa matendo na maneno Mwenyezimungu Amewaridhia na wao wamemridhia, lakini pamoja na yote hayo ALLAH katika kuukemea Ushirikina Alimwambia Mtume S.A.W Maneno yafuatayo.


وَلَقَدۡ أُوحِىَ إِلَيۡكَ وَإِلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكَ لَٮِٕنۡ أَشۡرَكۡتَ لَيَحۡبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ ٱلۡخَـٰسِرِينَ


''Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kukhasiri''. AZzumar 65.


Kwa mujibu wa aya hii ni kwamba mitume wote walielezwa kuwa atakaye mshirikisha mola wake basi amali zake zote zitaporomoka yani zitaharibika sasa ikiwa mitume ambao ni vipenzi wa ALLAH wanaambiwa hivyo je mimi na wewe?

katika Almaida :72    إِنَّهُ ۥ مَن يُشۡرِكۡ بِٱللَّهِ فَقَدۡ حَرَّمَ ٱللَّهُ عَلَيۡهِ ٱلۡجَنَّةَ وَمَأۡوَٮٰهُ ٱلنَّارُ‌ۖ

"kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni"

Sasa ndugu msomaji kuna jambo zuri kama mtu kupata pepo na ubaya ulioje kwa atakayeikosa pepo maana atakuwa na makazi ya kudumu motoni.

 
Miongoni mwa vitendea kazi vinavyotumiwa na washirikina

Baada ya kusoma hizo aya kutoka katika kitabu cha ALLAH ambacho ndio muongozo mkuu wa waislam utajifunza kuwa kumbe Uislam haukubaliani hata kidogo na ushirikina hivyo pindi atakapoonekana mtu yeyote mwenye nafasi au cheo chochote anayejinasibisha na uislam huku akisifika kwa ushirikina basi vitendo vya mtu huyo ahukumiwe navyo mwenyewe na sio uislam.


Leo tulikuwa tunaangalia kwa kifupi madhara ya Ushirikina yanayompata muhusika wa vitendo hivyo kwa muumba wake tumeona kuwa mtu huyo anapata hasara kubwa ya kuharibikiwa na vitendo vyake vyote na kubaki na madhambi makubwa kingine anayejihusisha na vitendo vya ushirikina wakati wengine wakipata nafasi maalum ya kuombewa siku ya hukumu yeye hatopata nafasi hiyo pia anaingia motoni kabla ya hesabu ya matendo ya waja haijaanza.

Hivyo nawasihi sana wasomaji wangu tujiepushe na vitendo vya kishirikina ili tusipate hasara kuu duniani na siku ya kiama.


Wiki ijayo Inshaa ALLAH tutaangalia sehem ya 2. ya somo hili ambapo litahusika na Madhara ya Ushirikina kijamii hapa duniani.

Ukiwa na Maswali,Maoni au ukihitaji kusomewa dua kwa ajili ya mambo mbalimbali nitafute kwa namba 0715604488.