KISA CHA MASIKINI CHENYE MAZINGATIO -1
Msomaji wangu Mpendwa,
Assalaamu alaykum,
Kama ilivyo wajibu wetu tuanze kwa kumshukuru Allaah ambaye ni Muumbaji na Mlezi wa Viumbe wote hafanani ya yeyote wala chochote kwa kutujaalia kuwa hai muda huu na kuweza kukumbushana mambo mbalimbali yahusuyo maisha yetu, pia nimtakie ziada ya rehma na amani Mtume Muhammad S.A.W na Aali zake na Sahaba zake na wote watakaowafuata kwa wema mpaka siku ya malipo.
Leo ndugu yangu nimependelea kukuletea simulizi hii ya watu watatu ambao walikuwa masikini lakini pia walikuwa na magonjwa mbalimbali na simulizi hii nainukuu kutokana na Hadithi ya Mtume S.A.W
Hadithi anaisimulia Abu hurayra (r.a) kuwa mtume s.a.w amesema:-
Watu watatu katika bani israil Mwenye ugonjwa wa ngozi, Mwenye matatizo ya kutoota nywele na kipofu Allah alitaka kuwapa mtihani, Akawapelekea Malaika,
Malaika akamwendea mwenye ugonjwa wa ngozi akamuuliza kitu gani unakipendelea Zaidi? akasema ngozi nzuri na rangi nzuri na iniondoke hii hali ambayo watu wamekuwa wakininyanyapaa kwayo , basi yule malaika akampangusa(akabadilika akawa na rangi nzuri na ngozi nzuri) kisha akamuuliza unapendelea mali gani? akasema ngamia, akapewa ngamia mwenye mimba ambaye alikuwa anakaribia kuzaa kisha akamwambia Allah akubariki katika ngamia huyu.
Kisha (Malaika) akamwendea aliyekuwa na matatizo ya kutoota nywele akamuuliza kitu gani unakipenda Zaidi? akasema napenda nywele nzurina iniondoke hii hali ambayo watu wamekuwa wakininyanyapaa kwayo , akampangusa ugonjwa ukamuondoka na akawa na nywele nzuri, kasha akamuuliza unapenda mali gani? akasema Ng'ombe nae akampa Ng'ombe mwenye mimba aliyekuwa anakaribia kuzaa kisha akamwambia Allah akubariki katika Ng'ombe huyu.
Kisha (Malaika) akamwendea kipofu akamuuliza kitu gani unakipenda Zaidi? akasema napenda Allaah anirudishie macho yangu ili nipate kuwaona watu basi yule Malaika akampangusha Allaah akamrudishia macho yake, Kisha akamuuliza unapenda mali gani? akajibu napenda Mbuzi (au Kondoo) Yule malaika akampa Mbuzi (au Kondoo) mwenye mimba aliyekuwa anakaribia kuzaa, akamwambia Allaah akubarik katika Mbuzi huyu.
Basi huyu Ngamia wakazaliana kwa wingi ikawa ana zizi kubwa la Ngamia na huyu Ng'ombe wakazaliana kwa wingi akawa na zizi kubwa la Ng'ombe na yule Mbuzi wakazaliana kwa wingi akawa na zizi kubwa la Mbuzi.
Inshaa Allaah tutaendelea na sehemu ya 2 ya simulizi hii yenye mazingatio
N.B kukionekena mapungufu kwenye tafsiri hii basi huko ndio kukamilika kwa sifa ya ubinaadamu na wala sio kusudi la Mwandishi hivyo nakaribisha masahihisho kutoka kwa wasomaji wangu ili kuboresha katika sehemu ya pili ya simulizi hii.
Mpendwa Msomaji wangu ili kupata haya na mengineyo nifuatilie kupitia twitter kwa kuponyeza hapa https://twitter.com/HemediPalike