FUNGA YA RAMADHANI NA MAELEKEZO YAKE-02

Ubora Wa Swaumu Na Faida Zake
A.      Ubora Wa Funga

Zinashuhudia ubora wa swaumu na kuthibitisha hadithi zifuatazo: kauli yake Mtume (S.a.w): “Funga ni kinga inayomkinga mtu na moto kama ilivyo ngao ya mmoja wenu inavyomkinga vitani” (Ameipokea Imam Ahmad na An Nasay)

 Na Kauli ya Mtume (S.a.w):
Mwenye kufunga siku moja tu Kwa ajili ya Allah, Allah atauepusha Uso wa mfungaji huyo na moto kwa siku hiyo kiasi cha umbali wa maili sabini”. (Ameipokea Attirmidhy,Anasay, Ibn Maajah na Imam Ahmad)

Na Kauli Yake Mtume (S.a.w): “Dua ya mfungaji hairejeshwi pindi atakapoomba pale anapofungua”. (Ameipokea Ibn Majah na A-lhakim)

Na kauli yake Mtume (S.a.w): “Hakika peponi kuna mlango unaoitwa Rayyaan, Wataingilia mlango huo siku ya kiama watu waliofunga tu,Hatoingilia mlango huo yeyote asiyekuwa mfungaji. Kutaulizwa wako wapi waliofunga watu watasimama hatoingilia mlango huo yeyote na wakimaliza mlango utafungwa na hatoingia katika mlango huo yeyote” (Imepokewa na Bukhari, Muslim na Annasay)

B.      Faida Za Funga
 
Funga ina faida za kiroho,Kijamii na za kiafya, nazo ni:

Miongoni mwa Faida Za Kiroho Za Funga ni kwamba funga inazoesha uvumilivu na inatia nguvu. Na Funga inafundisha kuidhibiti nafsi kusaidia. Na katika nafsi kunapatikana uwezo wa  kumcha Allaah na pia inalea mafsi malezi mazuri na khasa kumcha Allah ambayo ndio sababu kubwa ya funga kama ilivyokuja katika kauli yake Allah Mtukufu: “ Mmefaradhishiwa funga kama walivyofaradhishiwa walio kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”. (Albaqara:183)
 
Na Faida Za Swaumu Kijamii. 

 Ni kwamba umma unazoeshwa hali ya nidhamu na umoja na kupenda uadilifu na usawa na funga inatengeneza hali ya huruma na kutengeneza tabia kwa waumini kama ambavyo inahifadhi jamii na shari na mambo mabaya.
 

Na Miongoni mwa Faida Za Funga Kiafya

ni kwamba swaumu inasafisha  utumbo mdogo na inatengeneza utumbo wa chakula. Na inausafisha mwili Kutokana  na ziada ya vitu visivyotakiwa mwilini na vile vilivyogandia uliosababishwa na  mafuta na pia hupunguza athari za unene na katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Mtume (S.a.w): “Fungeni  Mtapata Afya”.

Itaendelea In Shaa Allah……


Msomaji Mpendwa ili kuyapata haya na mengineyo mengi tembelea duka la IBN HAZM MEDIA CENTER  lililopo Msikiti wa Mtoro Kariakoo, Dar Es Salaam ambao ni wasambazaji wa vitabu vya dini ya Kiislam vilivyotafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, Kiswahili na Kiingereza.