MLANGO WA TWAHARA-03
AINA ZA TWAHARA
Aina Za Twahara
Maulamaa wanaigawanya Twahara ya kisheria katika vigawanyo viwili:
1- Twahara ya kihakika:
Nayo ni Twahara ya kuondosha najisi. Hii inakuwa katika mwili, nguo
na mahala.
2- Twahara ya kihukumu:
Ni Twahara kutokana na hadathi, nayo inahusiana na mwili. Aina hii
ya Twahara ni sampuli tatu:
a). Tawahara kubwa, nayo ni kuoga,
b). Twahara ndogo, nayo ni
kutawadha, na badala ya viwili hivyo vinaposhindikana, inayofuata ni
c). kutayamamu.
KWANZA:TWAHARA YA KIHAKIKA
Makusudio ya najisi:
Najisi ni kinyume ya
Twahara. Na najisi (kilichonajisika), ni jina la kitu chenye kuonekana kichafu
kisheria. Ni lazima Muislamu ajiepusha nacho na akioshe kile kilichompata
katika kitu hicho
"Aina
Za Najisi"
Vitu ambavyo dalili ya kisheria imeonyesha juu ya unajisi wake ni:
1, 2- Kinyesi cha mwanadamu na mkojo wake
Na viwili hivi ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa.
Ama kinyesi, ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam)((Akikanyaga mmoja wenu kinyesi kwa kiatu chake, basi udongo
ndio kitwaharisho chake)). Pia zinaonyesha juu ya unajisi wake Hadiyth zote
zenye kuamrisha kustanji, na zitakuja karibuni.
Ama mkojo, ni kwa Hadiyth ya Anas kwamba bedui mmoja alikojoa ndani
ya msikiti, na baadhi ya watu wakamnyanyukia na kumwendea. Hapo Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:((Mwacheni msimkatishe)).
Akasema: Alipomaliza, aliagiza ndoo ya maji akaimimina juu yake (sehemu
iliyopatwa na mkojo).
3, 4- Madhii na wadii
Madhii:
Ni maji mepesi mno yenye kunatanata yanayotoka wakati wa matamanio
kama wakati wa kuchezeana (mke na mume), au kukumbuka kuingilia kimwili
(kufanya ngono) au kutaka kufanya. Maji haya hayachupi wala hayafuatiwi na
mchoko, na huenda mtu asihisi kutoka kwake. Humtoka mwanamume na mwanamke,
lakini kwa wanawake ni zaidi. Nayo ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa. Na
kwa ajili hiyo, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru
kuuosha utupu kwa kutoka maji hayo.
Katika Al-Bukhaariy na Muslim ni kwamba Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aliyemuuliza kuhusu madhii: ((Atauosha
uume wake na atatawadha)).
Ama wadii:
Hayo ni maji mazito meupe yanayotoka baada ya kukojoa. Ni najisi
kwa makubaliano (ijmaa) ya Maulamaa.
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas akisema:"Manii, wadii na madhii.
Ama manii, ni yale ambayo yakitoka, ni kuoga. Ama wadii na madhii, akasema:
Uoshe utupu wako – au nyuchi zako – na tawadha wudhuu wako wa Swalah".
5- Damu ya hedhi
Ni kwa Hadiyth ya Asmaa binti Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhuma),
amesema: "Alikuja mwanamke fulani kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mmoja wetu nguo yake
ikiingiwa na damu ya hedhi, afanyaje? Akasema Mtume:(((Ataipikicha, kisha ataikwangua
kwa ncha ya vidole na maji, kisha ataisuuza, na kisha ataswali nayo)).
6- Kinyesi cha mnyama ambaye nyama yake hailiwi
Imepokelewa toka kwa 'Abdullah ibn Mas'uud, amesema: Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kwenda haja kubwa akasema:
((Niletee mawe matatu)). Nilimpatia mawe mawili na kinyesi cha (punda).
Aliyachukua mawe mawili, akakitupa kinyesi na akasema: ((Hii ni najisi)).
Na kitendo hiki kimeonyesha kwamba kinyesi cha mnyama asiyeliwa
nyama yake ni najisi.
7- Mate ya mbwa
Hakika Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Kukitwaharisha chombo cha mmoja wenu anapokilamba mbwa ni kukiosha mara saba,
moja kati ya hizo kwa mchanga)).
Na bila shaka Hadiyth imeonyesha kwamba mate ya mbwa ni najisi.
8- Nyama ya nguruwe
Ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa kwa kuelezewa wazi katika
neno Lake Subhaana:
« Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu
kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu
inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu» [6:145]
9- Nyamafu
Nao ni mzoga wa mnyama aliyejifia mwenyewe bila ya chinjo la
kisheria. Ni najisi kwa ijmaa ya Wanazuoni kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Inapotiwa rangi ngozi ya nyamafu, basi
imetwaharika)).
Haviingii katika hukumu hii:
(a) Maiti ya samaki na nzige.
Kwani viwili hivi ni Twahara kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam):
((Tumehalalishiwa maiti
mbili na damu mbili. Ama maiti mbili ni samaki na nzige. Ama damu mbili ni ini
na wengu)).
(b) Maiti ya asiye na damu ya kuchuruzika
Kama vile nzi, nyuki, sisimizi, chawa na kadhalika kwa neno lake
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((Akiangukia nzi katika
chombo cha mmoja wenu, basi amzamishe wote au amtupe, kwani hakika katika bawa
lake moja kuna ugonjwa na katika jingine kuna ponya)).
(c) Mfupa wa mfu, pembe yake, kucha yake, manyoya yake na magoya
yake.
Hivi vyote asili yake ni Twahara. Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake
(1/342) ameeleza: Amesema Az-Zuhriy - kuhusu mifupa ya mzoga wa mnyama kama
vile tembo na wengineo - : Niliwakuta watu katika Maulamaa watangu wema
wakichania nywele na wakijitia mafuta kwa vitu hivyo, hawaoni kwa hilo ubaya
wowote.
10- Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai
Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai, kina hukumu ya nyamafu kwa
neno lake Mtume(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):((Kilichokatwa toka
kwa mnyama aliye hai, basi hicho ni nyamafu)).
11- Mabaki ya maji yaliyonywewa na mnyama mkali au mnyama asiye
mkali ambaye nyama yake hailiwi.
Unajisi wake unaonyeshwa na kauli yake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam alipokuwa akiulizwa kuhusu maji yanayokuwa jangwani
(nyikani), na yale yanayonywewa mara kwa mara na wanyama wakali au wasio wakali
akasema: ((Maji yakiwa kullatayni, hayabebi uchafu (najisi)).
Ama paka na walio chini yake, basi mabaki yake ni Twahara kwa neno
lake Mtume(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):((Hakika yeye si najisi,
bali ni katika wanaowazungukeni wa kiume na kike)).
12- Nyama ya mnyama asiyeliwa
Hii ni kwa Hadiyth ya Anas (Radhiya Allahu 'anhu) amesema:
"Tuliipata nyama ya punda – yaani siku ya Khaybar – na Mtume (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanadi: ((Hakika Allaah na Mtume Wake
Anakukatazeni nyama ya punda, kwani hakika ni uchafu)) (najisi).
Na kwa Hadiyth ya Salamah bin Al Akwa'a, amesema: Ilipoingia jioni
ya siku waliyofunguliwa Khaybar, waliwasha mioto mingi. Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Moto huu ni wa nini? Mmeuwashia kwa
jambo gani?))Wakasema: "Kwa nyama". Akasema: ((Kwa nyama ya nini?)).
Wakasema: Kwa nyama ya punda wa mjini. Akasema: ((Imwageni na kivunjeni)).
Akasema mtu mmoja: Ewe Mtume wa Allaah! Je, tuimwage na tukioshe? Akasema: ((Au
hilo)).
Katika Hadiyth hizi mbili, kuna dalili juu ya unajisi wa nyama ya
punda wa mjini (kienyeji) kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) katika Hadiyth ya kwanza: ((Kwani hakika ni uchafu)) (najisi), na
katika Hadiyth ya pili kwa kukivunja chombo kwanza, kisha kuruhusu kutumika kwa
kukiosha mara ya pili.
"Je,
Manii Ni Twahara Au Najisi?"
Wanazuoni wametofautiana katika hilo juu ya kauli mbili:
Kauli ya kwanza:
Inasema kwamba manii ni najisi. Kauli hii ameisema Abu Haniyfah na
Maalik. Nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo
kwa Hadiyth ya 'Aaishah alipoulizwa kuhusu manii yaliyoingia katika nguo
akasema:
"Nilikuwa nikiyaosha kwenye nguo ya Mtume wa Allaah (Swalla
Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha yeye hutoka moja kwa moja kwenda
kuswali huku athari ya doa la maji ikiwa katika nguo yake".
Na kuosha hakuwi ila kwa kitu kilicho najisi.
Kauli ya pili:
Wenye kauli hii wamesema kuwa manii ni Twahara. Kati ya waliolisema
hilo ni Ash-Shaafi'i na Daawuud Hii ni riwaya sahihi zaidi kati ya riwaya mbili
iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah
kuhusu manii, amesema:"Nilikuwa nikiyakwangua toka katika nguo ya Mtume
(Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)"
Na kwa Hadiyth yake vile vile kwamba mgeni alishukia kwa 'Aaishah
na akawa anaiosha nguo yake. 'Aaishah akamwambia: "Bila shaka ilikuwa
inakutosha ikiwa utayaona, uoshe mahala pake, na ikiwa hukuyaona, basi
utanyunyizia maji kuzungukia hapo. Na bila shaka umeniona nikiyakwangua
mkwanguo mmoja toka katika nguo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) na yeye akaiswalia".
Na kutosheka kukwangua, kunaonyesha juu ya utwahara wake.
Wenye kusema kuwa ni najisi, wamejibu kuwa kukwangua hakuonyeshi
kuwa manii ni Twahara, bali kunaonyesha namna ya kutwaharisha kama inavyokuwa
katika kuvitwaharisha viatu kwa kuvipangusa katika mchanga.
Hili linajibiwa kwa kusema kuwa 'Aaishah kuyakwangua manii mara hii
na kuyaosha mara nyingine, hakuhukumii unajisi wake, kwani nguo inaoshwa kwa
kuingiwa na makamasi, mate na uchafu. Na hivi ndivyo walivyosema Maswahaba
wengi kama vile Sa'ad bin Abi Waqqaasw, Ibn 'Abbaas na wengineo:
"Bila shaka manii ni
kama makamasi na mate, jisafishe nayo japokuwa kwa kijiti."
Na kwa hili, imedhihiri kuwa kitendo cha 'Aaishah (Radhiya Allahu
'anhaa) si jingine bali ni katika mlango wa kuchagua (namna ya) usafi.
Hukumu ya utwahara wa manii inapata nguvu kwamba Maswahaba walikuwa
wakiota wakati wa enzi ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na
kwamba manii ilikuwa ikiingia katika mwili wa mmoja wao na nguo yake. Na hili
ni kati ya matatizo makubwa. Na lau kama yangelikuwa ni najisi, basi ingelikuwa
ni lazima kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaamrishe
wayaondoshe kama alivyowaamrisha wastanji. Na hakuna yeyote aliyelinukuu hili,
na kwa hivyo imejulikana kwa yakini kuwa kuyaondosha hakukuwa ni jambo la
lazima.
Hivyo basi Manii Yanabaki kuwa ni Twahara
Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.